Shirika la Kikundi cha Huduma Majumbani
Mkoa wa Mbeya(KIHUMBE) limeanzisha kituo cha Vijana katika Kata ya Forest
(Foresti ya zamani) Jijini Mbeya.
Meneja wa Kihumbe, Ptolemy Samwel,
alisema lengo la kuanzishwa kwa kituo hicho ni kutokana na vijana wa kike na
kiume kuathirika zaidi na maambukizi ya Ukimwi na kukosekana sehemu maalumu ya
kuwakutanisha na kupewa elimu.
Alisema Shirika la Kihumbe
limeanzisha kituo maalumu cha vijana baada ya kuona vijana wengi jijini hawana
sehemu ya kukutana na kujadili matatizo yao iliona ni muhimu kuwepo kwa kituo
cha vijana ambacho pia watatumia kujadili njia mbali mbali za utekelezaji wa
mkakati wa kuzuia maambukizi ya VVU/UKIMWI.
Aliongeza kuwa kutokana na ukosefu wa
ajira kituo kiliamua kuwawezesha vijana kwa kuwapatia elimu ya ujasiliamali
kupitia vikundi vyao vilivyopo katika Kata mbali mbali za jijini Mbeya ili
kuwawezesha kujua fursa zilizopo na kuweza kuzitumia ili waweze kujiajiri
wenyewe.
Alizitaja shughuli zitakazotolewa katika
kituo hicho kuwa ni pamoja na kutoa elimu ya VVU/UKIMWI kwa njia za sinema,
Elimu ya matumizi sahihi ya kondomu, magonjwa ya ngono, mtandao wa ngono, ngono
mtambaluka na ugawaji wa kondomu.
Aliongeza kuwa shughuli zingine zitakuwa
ni kutoa huduma za ushauri nasaha na upimaji wa virusi vya ukimwi kwa hiari,
huduma ya daktari, michezo mbali mbali ya ndani ya kituo na nje, elimu ya
ujasiliamali pamoja na Msaada wa masomo kwa njia ya mtandao.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la
Mbeya, Dk Samwel Lazalo, amelipongeza shirika la Walter Reed Program(WRP)
linalomilikiwa na watu wa Marekani lenye makao makuu mkoani Mbeya kwa kufadhili
miradi inayowanufaisha wakazi wa jijini hapa.
Pongezi hizo alizitoa alipokuwa
akizindua kituo cha vijana kinachomilikiwa na kikundi cha Huduma majumbani Mkoa
wa Mbeya(KIHUMBE) kilichojengwa chini ya ufadhili wa Shirika la WRP
kilichopo Forest ya Zamani jijini hapa.
Alisema msaada wa ujenzi huo
utawanufaisha zaidi vijana wengi wa Jiji la Mbeya na wageni watakao tembelea
kwa kufundishwa maarifa mbali mbali pamoja na elimu juu ya maambukizi ya Virusi
vya Ukimwi.
Alitoa wito kwa vijana na wamiliki wa
kituo hicho kuhakikisha wanatumia kama ilivyokusudiwa ili kuwafurahisha walipa
kodi wa Marekani ambao ndiyo waliotoa ufadhili kupitia shirika lao la WRP kwa
vijana kutumia kupata maarifa mbali mbali yatakayowasaidia katika maisha.
Mkurugenzi huyo aliongeza kwa kuwataka
Viongozi wa Serikali katika ngazi ya kata na Jiji sehemu kilipojengwa kituo
hicho kuhakikisha wanaunga mkono jitihada za KIHUMBE na WRP ili kupata malengo
yanayotarajiwa kutokana na kituo hicho.
Na Mbeya yetu
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni