UONGOZI wa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya
kupitia kitengo cha Ustawi wa jamii umemtafutia kituo cha kulelea watoto
wa mitaani cha Nuru Ophans Centre Mama aliyejifungua mapacha wanne na kubakia
wawili baada ya kuugua Nimonia kwa ajili ya uangalizi wa karibu.
Hatua hiyo imekuja baada ya uongozi wa
Hospitali hiyo kumfuata mama mwenye watoto hao Aida Nakawala(25) pamoja na
mapacha wake waliobaki kutoka kijijini kwao Chiwanda Wilaya ya Momba mkoani
hapa na kuwalaza hospitalini hapo kwa uangalizi wa karibu kwa muda wa zaidi ya
wiki moja.
Aidha baada ya afya za watoto hao
kuimarika kwa kiwango kikubwa pia Uongozi wa Hospitali hiyo imemtafutia hifadhi
katika kituo cha kulelea watoto wa mitaani cha Nuru kilichopo Uyole jijini
Mbeya kwa ajili ya uangalizi wa karibu kutoka kwa wauguzi na maafisa wa ustawi
wa Jamii kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mbeya.
Akizungumza na waandishi wa habari
wakati akiwakabidhi watoto hao pamoja na mama yao kwenye uongozi wa kituo cha
Nuru Orphans centre, Katibu wa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, Aisha Mtanda,
alisema wameguswa na mazingira anayoishi mama huyo na kuamua kumpa uangalizi
kwa miezi sita zaidi.
Alisema jukumu hilo halipaswi kufanywa
na Hospitali kwa kuwa tayari walikuwa wamemaliza jukumu lao la kumhudumia
alipokuwa ana matatizo lakini wamelazimika kubeba jukumu hilo baada ya kuguswa
na mazingira na hali ya makazi ya familia hiyo.
Alisema Hospitali imekubaliana na
uongozi wa Kituo cha Nuru kwamba apewe hifadhi mama huyo na watoto wake ili
apate uangalizi wa karibu ikiwa na lengo la kunusuru maisha ya watoto waliobaki
kutokana na wengine kupoteza maisha kiuzembe kwa ugonjwa wa Nimonia.
Aliongeza kuwa Hali ya hewa ya Mkoa wa
Mbeya kwa siku zijazo kunakuwa na baridi kali sana hivyo watoto wasipokuwa
kwenye uangalizi wa karibu wanaweza kupatwa na ugonjwa wa Nimonia tena kwa
kukosa matunzo kama ya awali.
Kwa upande wake, Meneja wa Kituo cha
Nuru, Amanda Fihavango alisema alikubali jukumu la kuwapokea watoto hao pamoja
na mama yao kutokana na kuguswa na hali iliyowakuta ya kupotea kwa watoto
wawili kati ya wanne.
Aliongeza kuwa ingawa anakabiliwa na
changamoto nyingi zikiwemo za kiuchumi atajitahidi kwahudumia kadri ya uwezo
wake na kuomba wasamaria wema watakaoguswa na jambo hilo kujitolea kwa hali na
mali kufanikisha kuokoa uhai wa watoto hao pamoja na wengine anaowalea.
Alisema kituo chake hupokea watoto
waliookotwa baada ya kutupwa na wazazi wao au mama zao kufariki mara baada ya
kutoka kujifungua ambao hupelekwa na Serikali kupitia Ustawi wa Jamii ingawa
haichangii fedha zozote baada ya kuwapeleka.
Mtu yoyote mwenye kuguswa anaweza
kuwasilisha mchango wake kituoni hapo au kuwasiliana na Meneja wa Kituo cha
Nuru kupitia namba za Simu 0754 043004 kwa ajili ya kusaidia
watoto hao pamoja na mama yao kuishi hapo kwa muda wa miezi sita.
imechapishwa na clever julius
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni